Kama Ulimis Historia Fupi ya Msanii Diamond Platnumz Iko Hapa.
Mkali wa Bongo fleva, Nasibu Abdul au maarufu kwa jina la Diamond akipozi.
ANAITWA Nasibu Abdul au maarufu kwa jina la Diamond. Alizaliwa saa kumi na moja jioni ya Oktoba 2, 1989 katika Hospitali ya Amana iliyopo Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam. Wazazi wake walimpa jina la Nasibu wakiamini ni la bahati.
Diamond aliongea hivi karibuni na safu hii ya Mjue Huyu ambapo aliweka wazi mambo mengi ya maisha yake. Diamond akiwa hajapata ufahamu, yaani bado mdogo, wazazi wake walitengana kwa sababu ambazo bado hazijawa wazi na baba yake kumuacha na mama.
Kufuatia hali hiyo, ilibidi mama yake ahamie kwa mama yake mzazi (bibi wa Diamond), Tandale Magharibi, Dar. Hapo ndipo yakawa makazi ya mama huyo na mwanaye.
Mnamo mwaka 1995, Diamond alianza elimu ya awali katika Shule ya Chakula Bora iliyopo Tandale- Uzuri. Mwaka 1996 alianza elimu ya msingi katika Shule ya Msingi Tandale- Magharibi iliyopo jijini Dar es Salaam.
Mwaka 2000, Diamond akiwa darasa la tano alianza kupenda muziki, hivyo akawa anakopi baadhi ya nyimbo za wasanii waliokuwa wakihiti ndani na nje ya Bongo na kuimba yeye katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam. Kwa kuliona hilo, mama yake alianza kumnunulia kanda za albamu za wasanii tofauti hata kumwandikia baadhi ya nyimbo za wasanii hao ili mwanae aweze kuzishika na kuimba kirahisi.
Diamond alizidi kuupenda muziki ikabidi mama yake awe anampeleka kwenye matamasha mbalimbali ili mwanae apate nafasi ya kuimba.
Baadhi ya ndugu walimjia juu mama huyo wakidai anamharibu mtoto badala ya kumuhimiza masomo anamwingiza kwenye muziki ambao walidhani haukuwa na faida yoyote.
'Diamond Platinumz'
“Kusema ukweli pamoja na yote hayo, hali ya maisha ilikuwa si nzuri kwa mama maana hakuwa na kazi ya maana wala vyanzo vikubwa vya fedha, hivyo ilibidi atumie kiasi kidogo alichokipata kutoka kwenye kodi ya vyumba viwili alivyopewa na bibi ili kunisomesha,” alisema Diamond.
CHUMBA KIMOJA NA MAMA
Diamond aliendelea kusema kuwa, kutokana na kupangisha vyumba viwili ilibidi yeye na mama yake kuhamia kwenye chumba cha bibi yake na maisha yakaendelea humo.
AMALIZA SHULE YA MSINGI
Mwaka 2002, Diamond alimaliza masomo ya elimu ya msingi lakini ili aende sekondari, mama yake alimwambia aachane na habari ya muziki azingatie masomo aweze kupata elimu itakayomsaidia mbele ya safari katika maisha.
AFANYA MUZIKI KWA SIRI
Nyota huyo aliendelea kusema kuwa akiwa sekondari, aliendelea kuimba muziki lakini kwa siri kubwa ili mama yake asijue.
Mwaka 2004, anasema alianza kuandika nyimbo zake mwenyewe kwa kuwa akili bado ilimwambia mafanikio yake yatapatikana huko.
AFANYA VIBARUA APATE PESA
Mwaka 2006, Diamond alimaliza elimu ya sekondari na kuanza kuimarisha ndoto yake ya kuwa mwanamuziki.
Alikuwa hana kazi ya kufanya nyumbani hivyo alianza kutafuta vibarua mbalimbali vya kumuwezesha kupata riziki ya siku. Miongoni mwa kazi hizo ni kuuza mitumba, kuweka mafuta kwenye magari (vituo vya mafuta), kupiga picha, kupigisha simu na kazi za kwenye viwanda mbalimbali.
CodeNirvana