Nimegundua Mpenzi Wangu Ni Fisadi Wa Mapenzi.












Shangazi nimegundua kuwa mwanamume tunayependana ni mwizi na nimeona ni heri nimuache. Lakini anashikilia kuwa ananipenda na hayuko tayari kuniacha. Nifanye nini?
Kupitia SMS

Ni hatari kujihusisha na mtu mhalifu kwani anaweza kukuweka mashakani. Ni bahati kwamba umegundua mapema kwamba mpenzi wako si mtu mzuri. Hata kama anakupenda hawezi kukulazimisha kuwa naye kwa hivyo vunja uhusiano huo haraka iwezekanavyo.

ANATAKA NIENDE KWAKE LAKINI NINAOGOPA

Kwako shangazi. Nimekuwa na uhusiano na kijana fulani kwa mwaka mmoja sasa. Amekuwa akinisukuma niende kwake lakini naogopa. Je, anaweza kuwa na nia mbaya kwangu?
Kupitia SMS

Kama hujawahi kuona dalili zozote mbaya kwake katika muda ambao mmekuwa pamoja, sioni ni kwa nini uwe na wasiwasi kwani ni jambo la kawaida kwa marafiki na wapenzi kutembeleana. Hata hivyo kuwa mwangalifu, kuna watu vigeugeu.

ANA MPENZI WA KANDO WANAYEWASILIANA NAYE

Kuna mwanamke mchumba wangu ambaye nimepanga kumuoa. Lakini nimepata ujumbe wa kimapenzi kwa simu yake ambao amemtumia mwanamume mwingine. Nishauri.
Kupitia SMS

Hizo ni dalili za mtu ambaye si mwaminifu. Fuatilia jambo hilo ujue huyo mwanamume ni nani na uhusiano uliopo baina yao. Ukijua ukweli utafanya uamuzi unaofaa.

TULIJUANA FACEBOOK.

Shikamoo shangazi? Kuna msichana tuliyejuana kupitia kwa facebook na anataka tuwe wapenzi. Je, ni sawa?
Kupitia SMS

Uhusiano wa dhati hujengwa kupitia watu kujumuika kwa muda na kujuana vizuri. Sidhani unaweza kumpenda mtu ambaye mnawasiliana tu kwa facebook wala hamjakutana. Kutana naye na ujipe muda wa kumsoma na kupima hisia zako kwake ndipo ufanye uamuzi unaofaa.

ANA WAPENZI WENGI

Kuna kijana ninayempenda lakini ana wasichana wengi sana. Yeye pia ananiambia ananipenda. Naomba ushauri wako shangazi.

Kupitia SMS

Hiyo ni hatua hatari unayotaka kuchukua kwa kuzisingizia mapenzi. Nashangaa kwamba unasema unampenda kijana huyo ilhali unajua ana wasichana wengi. Bila shaka anamdanganya kila mmoja kwamba anampenda. Kama umekubali kuingia kwenye mtego huo hiyo ni shauri yako.

AMEKATAA KUNIGAWIA TUNDA

Shikamoo shangazi. Kuna msichana ninayempenda naye pia anadai ananipenda lakini amekataa kabisa kunigawia tunda. Nafikiria kumuacha. Nishauri.
Kupitia SMS

Nashuku iwapo unampenda msichana huyo kama unavyodai na inaonekana unalenga tu hilo tunda. Mapenzi ya kweli huwa na subira na kila jambo lina wakati wake. Kama huwezi kusubiri, basi utaamua mwenyewe.

NIMETAFUTA NIKAKOSA
Hujambo shangazi? Nina umri wa miaka 24 na nimetafuta mpenzi sana lakini sijapata. Sasa nimechoka, naomba ushauri wako.
Kupitia SMS




Ukisema umechoka hiyo ina maana kwamba umeamua kuishi bila mpenzi kwa hivyo sijui unataka nikusaidie namna gani. Iwapo bado una nia endelea kutafuta kwani atafutaye hachoki.


NINA VIRUSI NA BADO SIJAOA

Shangazi mimi ninaugua Ukimwi na bado sijaoa. Nifanyeje?
Kupitia SMS

Huenda haitakuwa rahisi kwako kupata mwanamke aliye tayari kuolewa nawe kama yeye mwenyewe ni mzima wa afya. Hata hivyo, unaweza kutafuta aliye katika hali sawa na yako. Kila la heri. Unaweza kutumia ukumbi wa 'Uko Wapi?’ katika gazeti la Taifa Jumapili kutafuta. Maelezo hupatikana ukurasa wa 25 wa gazeti hilo.

DADAKE PIA NI MPENZI WANGU

Shangazi nina mpenzi ambaye dada yake ni rafiki yangu mkubwa. Sasa dada yake ameniambia mpenzi wangu amemtambulisha mwanamume mwingine kwake na akamsihi asiniambie. Nimemuuliza lakini amekana na kukasirika. Hata amekosana vibaya na dada yake. Nifanyeje?
Kupitia SMS

Kuna usemi kuwa panapofuka moshi pana moto. Labda msichana huyo amepata mwingine na sasa ameamua kuvunja uhusiano wenu. Hakutarajia pia dada yake angekwambia. Lakini kama amekana, hakuna unaloweza kufanya ila kusubiri uone mambo yatavyoenda. Ushauri wangu ni kwamba uwe tayari kwa lolote lile.

HANISAIDII KULEA

Shangazi mimi ni mama ya mtoto mmoja lakini mwanamume tuliyezaa naye hashughuliki kuhusu malezi ya mtoto. Kuna mwingine anayenipenda na yuko tayari kunioa pamoja na mtoto wangu. Naomba ushauri wako.
Kupitia SMS

Nijuavyo ni kuwa wanaume walio tayari kuoa mwanamke aliye na mtoto wameadimika sana siku hizi. Kama umempata aliye tayari kukuoa na unampenda basi una bahati sana, achana na maswali mengi na umnyakue kabla hajanyakuliwa uachwe ukijuta.





Newer Posts Older Posts
© Copyright WCB Daily Published.. Blogger Templates
Back To Top